Urasimishaji wa Ujuzi (RPL)

Utangulizi

Urasimishaji wa Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL) ni mchakato wa kutambua kutathmini na kuthibitisha ujuzi wa mtu bila kujali jinsi alivyopata ujuzi, lini na kwa muda gani na wapi ujifunzaji umefanyika.

Hatua za uthibitishaji wa ujuzi na utunuku wa cheti kwa mwanagenzi (Fundi aliyejifunzia mahali pa kazi pasipo kupita kwenye mfumo rasmi wa mafunzo) hufanywa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa vya moduli na sifa kamili za Miongozo ya utoaji na tathminini ya Elimu ya Ufundi Stadi. Kwa kuzingatia hili, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) huandaa na kutoa miongozo ya tathmini kwa moduli zinazotambulika Kitaifa.

Walengwa Wa Programu

Walengwa wa Programu hii ya RPL ni mafundi wenye ujuzi uliopatikana kupitia mafunzo yasiyo rasmi na ujuzi uliopatikana kupitia uzoefu wa maisha au kazi. Mwombaji wa programu ya RPL anaweza kutoka katika sekta rasmi ya uchumi au katika sekta isiyo rasmi.

Manufaa Ya Kurasimisha Ujuzi Kupitia Programu Ya RPL

Programu ya Urasimishaji wa Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL) inamuwezesha fundi aliyejifunza nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kuwa na sifa inayotambulika kitaifa na inayoaminika kwa waajiri na sekta mbalimbali ikiwemo Elimu na taasisi za kifedha. Hivyo huleta manufaa mengi, ikiwa ni pamoja na:

  1. Fundi asiye na cheti anawezeshwa kupata elimu na mafunzo rasmi yaliyoratibiwa na kukuza ujifunzaji kwa maisha yote.

  2. Fundi aliyerasimisha ujuzi anaweza kupata fursa ya kupata kazi bora zaidi, kuhamia kwenye uchumi rasmi au kufuzu kufanya kazi kama mtaalamu.

  3. Programu hii inamuwezesha fundi aliyepata ujuzi nje ya mfumo rasmi wa Elimu kukidhi sifa za kutuma maombi ya zabuni za serikali na huduma za kifedha kwa biashara.Hivyo kuboresha uwezo wake kibiashara.

  4. Programu hii inamuwezesha mwanagenzi kuboresha mazingira yake ya kazi, kupata ajira zenye staha na heshima awapo kazini na katika jamii kwa ujumla.

  5. Programu hii inamuwezesha mwanagenzi kuboresha ujuzi na kuongeza umahiri katika fani yake. Hivyo kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa zake.

  6. Programu hii inasaidia kuinua tija mahala pa kazi na kusaidia waajiri/wenye makampuni kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu.

Sifa Gani Unapaswa Kuwa Nazo Ili Uweze Kurasmisha Ujuzi Kupitia Programu Ya RPL?

  1. Mwombaji awe na ujuzi wa ufundi ambao aliupata bila kupitia chuo au mfumo rasmi wa mafunzo. Hivyo hana cheti kinachoelezea kuhusu ujuzi alionao.

  2. Mwombaji awe na uzoefu usiopungua miaka mitano (5) kwenye fani yake.

  3. Mwombaji awe Mtanzania mwenye umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 45.

  4. Ujuzi anaoomba kurasimisha uwe miongoni mwa fani ambazo VETA inazirasimisha kwa wakati huo. Fani hizo zimeainishwa katika kipengele kinachofuata.

Orodha Ya Fani Unazoweza Kurasimisha Ujuzi Wako Kupitia Programu Ya RPL Kwa Sasa

Kwa sasa waombaji wanaoweza kurasimisha ujuzi kupitia Programu ya RPL wanapaswa kutoka katika fani zifuatazo:

  1. Uashi

  2. Uselemara

  3. Ufundi Magari (Makenika)

  4. Upishi

  5. Uhudumu wa Hoteli, Baa au Migahawa

  6. Ufundi Uungaji Vyuma (Welding)

  7. Ufundi Cherehani (Ushonaji wa Nguo)

  8. Ufundi Bomba

  9. Ufundi wa Umeme wa Najumbani na

  10. Ufundi wa Kunyoosha bodi za Magari

VETA inatarajio kuongeza orodha ya fani kulingana na mahitaji. Mwombaji mwenye ujuzi zaidi ya fani moja anapaswa kuchagua fani moja kwa wakati.

Hatua Za Kufuata Ili Kurasimisha Ujuzi Wako

Ikiwa mwombaji anakidhi vigezo vilivyotajwa hapo juu ataendelea na hatua za uombaji kama ifuatavyo:

  1. Kujaza fomu ili kuomba kurasimisha umahiri wake.

  2. VETA itamtaarifu muda na sehemu atakayofanyiwa tathmini ya ujuzi wake. (Endapo amekidhi vigezo)

  3. Mwanagenzi atastahili kupewa cheti endapo ameweza kuthibitisha umahiri wake katika fani na maeneo aliyotathminiwa.

  4. Endapo mwanagenzi atafaulu zoezi la tathmini ya ujuzi, atapewa mafunzo maalumu yasiyozidi siku 14 ili kuziba mapungufu yaliyobainika wakati wa kutathminiwa ujuzi wake.

  5. Baada ya programu ya kuondoa mapungufu kukamilika, mwanagenzi aliyefaulu atatunukiwa cheti cha moduli cha ufundi stadi katika fani yake.

VETA inatarajio kuongeza orodha ya fani kulingana na mahitaji. Mwombaji mwenye ujuzi zaidi ya fani moja anapaswa kuchagua fani moja kwa wakati.

Mafanikio

  1. Tangu kuanza kwa mpango huu (mwaka 2012), jumla ya wanagenzi 21,000 wamefanyiwa tathmini na kutunukiwa vyeti.

  2. Wanagenzi wengi waliorasimishwa wamepata manufaa mbalimbali ikiwemo kurasimisha shughuli zao (kwa kusajili makampuni); kushindana katika zabuni na kupata kazi kwenye taasisi za umma na wale waliokuwa wanafanya kazi kama vibarua wameajiriwa rasmi.